Saturday 8 February 2025 - 19:26

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mwanzoni mwa mkutano huo, Bwana Mohammad Ismail Darwish, Mkuu wa Baraza la Uongozi la Hamas, alipongeza ushindi mkubwa wa Muqawamah wa Ghaza na kumwambia Kiongozi wa Mapinduzi, kwamba: Tunazingatia kusadifiana kwa siku za Ushindi wa Muqawamah wa Ghaza na kumbukumbu ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na tuna matumaini kuwa kusadifiana huku ni msingi maandalizi ya Ukombozi wa Quds na Msikiti wa al-Aqsa.

Mwanzoni mwa kikao hicho, Bwana Khalil Al-Hayya, Naibu wa Rais (Mkuu) wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amempongeza Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Ushindi wa Muqawama wa Ghaza na kusema:

"Leo tumekuja kukutana na Mheshimiwa, sote tunajivunia ushindi huu mkubwa na kwamba ni ushindi wa pamoja baina yetu na wa Jamhuri ya Kiislamu."

Katika mkutano huu, Ayatollah Khamenei vile vile amethamini na kuonyesha heshima ya kuwakumbuka Mashahidi wa Ghaza na Makamanda waliouawa Kishahidi wa Palestina hususan Shahidi Ismail Haniyyah, ambapo aliwahutubia viongozi wa Hamas na kusema: Mwenyezi Mungu amekupeni nyinyi na watu wa Ghaza Utukufu na Ushindi, na akaifanya Gaza kuwa ni mfano halisi wa Aya Tukufu inayosema:

"Huenda kundi dogo likalishinda kundi kubwa na lenye nguvu kwa taufiki na idhini ya Mwenyezi Mungu".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Nyinyi mliushinda utawala haram wa Kizayuni na kwa hakika na kiuhalisia mmeishinda Marekani, na kwa Fadhila na Neema ya Mwenyezi Mungu hamkuwaruhusu kamwe waweze kuyafikia malengo yao yoyote yale.

Ayatollah Khamenei, akiashiria mateso ambayo watu wa Ghaza waliyastahimili katika mwaka mmoja na nusu wa Upinzani(Muqawamah), alibainisha akisema kuwa: Mateso na gharama zote hizi, matokeo na hatimaye yake imekuwa ni Ushindi wa Haki dhidi ya Batili, na watu wa Ghaza wakawa ni mfano hai kwa wale wote ambao nyoyo zao ziko katika (Mapambano ya) Upinzani (Muqawamah).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru timu ya wafanya mazungumzo ya Hamas na kuyataja mafanikio ya mapatano hayo kuwa makubwa na akasema: Leo, ni wajibu wa ulimwengu mzima wa Kiislamu na waungaji mkono wote wa Muqawamah kuwasaidia watu wa Ghaza ili kupunguza mateso na maumivu yao.

Ayatollah Khamenei ametaja kuwa kuna haja ya kupanga mipango kwa ajili ya shughuli za kiutamaduni na kuendeleza njia ya sasa ya shughuli za kipropaganda (kitablighi) pamoja na masuala ya kijeshi na ujenzi mpya wa Ghaza, na akaongeza kuwa: Majeshi ya Muqawamah na Hamas yalifanya vyema sana katika kazi za Propaganda (Tablighi) na vyombo vya habari, na njia hii inapaswa kuendelezwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliichukulia Imani kuwa ndio kigezo kikuu na silaha isiyo na kipimo ya Muqawamah dhidi ya adui na akasema: Ni kwa sababu ya imani hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu na Mkondo wa Mapambano ya Muqawamah, hawahisi kamwe kuwa dhaifu dhidi ya maadui.

Ayatollah Khamenei akiashiria vitisho vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wananchi wa Iran amesisitiza kuwa: Vitisho hivyo havina taathira yoyote katika fikra za Taifa na Viongozi wetu, na pia wanaharakati na vijana wa nchi hii.

Ameashiria kuwa suala la kuihami Palestina na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina halina nafasi ya kutiliwa shaka katika fikra za wananchi wa Iran na suala hilo limetatuliwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Suala la Palestina ni suala kubwa kwetu sisi, na Ushindi wa Palestina pia ni suala la uhakika kwetu sisi.

Ayatollah Khamenei amesisitiza kuwa, hatimaye ushindi wa mwisho utakuwa wa Wananchi wa Palestina, na akabainisha: Matukio na misukosuko havipaswi kusababisha (kuleta) shaka, bali kila mtu anapaswa kusonga mbele kwa nguvu ya imani na matumaini ya kupata (sapoti na) msaada wa Mwenyezi Mungu.

Mwishoni, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwaambia viongozi wa Hamas: "Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, siku itafika ambapo nyote mtakuwa mmelitatua suala la Quds kwa ulimwengu wa Kiislamu na kwa fahari kubwa, na bila shaka siku hiyo itatokea."

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha